Ticker

6/recent/ticker-posts

MZABIBU WA KWELI By Askofu Zachary Kakobe


MZABIBU WA KWELI


ZACHARY KAKOBENeno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        
Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org
SIKU YA KUICHAMBUA BIBLIA
SOMO:  MZABIBU WA KWELI
K
atika kuzidi kuendelea kujifunza Kitabu cha YOHANA katika Biblia zetu, leo, tunaanza kuichambua SURA ya 15 ya Kitabu hiki, na hususan leo, tutajifunza YOHANA 15:1-8.  Katika mistari hii, pamoja na mambo mengine, tunajifunza juu ya “MZABIBU WA KWELI“.  Tutayagawa mafundisho yote tunayoyapata katika mistari hii katika vipengele kumi na moja:

(1)   MZABIBU WA KWELI (MST. 1);
(2)   MUNGU BABA, MKULIMA (MST. 1);
(3)   SISI NI MATAWI (MST. 5);
(4)   KILA TAWI LINAPASWA KUZAA MATUNDA (MST.2);
(5)   KUNGOLEWA KWA TAWI LISILOZAA (MST. 2,6);
(6)   KUSAFISHWA KWA TAWI LIZAALO (MS. 2);
(7)   KUSAFISHWA KWA NENO LA MUNGU (MST. 3);
(8)   PASIPO YESU, SISI HATUWEZI KUFANYA NENO LOLOTE (MST. 4-5);
(9)   SIRI YA KUJIBIWA MAOMBI (MST. 7);
(10) KUZAA SANA HUMTUKUZA BABA (MST. 8);
(11) KUZAA SANA, ALAMA HALISI YA MWANAFUNZI WA YESU (MST. 8).

(1)                           MZABIBU WA KWELI (MST. 1)
Yesu Kristo, anajitaja hapa kwamba ni Mzabibu wa Kweli.  Mzabibu wa Uongo au usio halisi ni upi?  Wana wa Israeli, wanatajwa pia kwamba ni mzabibu uliotolewa Misri, na kupandwa Kanaani, baada ya mataifa kadha kufukuzwa katika nchi ya Kanaani (ZABURI 80:8).  Baada ya kuupanda mzabibu huu, Mungu alitumaini kwamba mzabibu huu ungezaa zabibu za kweli, lakini kinyume chake, ulizaa zabibu mwitu; kwa maana kwamba Wana wa Israeli kwa kukosa shukrani, walifanya mambo yasiyo ya haki, yasiyompendeza Mungu na kuishi kinyume kabisa na Neno la Mungu, kwa unafiki mwingi wa Mafarisayo na Masadukayo, wa kujiosha nje tu (ISAYA 5:1-2,7; yeremia 2:21-22).  Hatimaye Yesu Kristo naye alipandwa Kanaani.  Yeye alikuwa Mzabibu wa Kweli uliozaa zabibu njema maana aliishi maisha yaliyompendeza Baba hata kutoka mbinguni Baba alisema, “Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye“.  Hapa angeweza pia kusema, “Huyu ni Mzabibu wa kweli ninaopendezwa nao“.
(2)                          MUNGU BABA, MKULIMA (MST. 1)
“Ulileta mzabibu………ukaupanda“(ZABURI 80:8).  Mwenye kuupanda, ni Mungu Baba.   Baba pia, ndiye aliyemtoa Mwana wake wa pekee Yesu, akampanda katika mwili wa mwanadamu, duniani.  Tunajifunza jambo kubwa hapa.  Mungu Baba, ni Mkulima.  Ukulima, ni kazi ngumu.  Baba, ni mchapakazi.  Hatuwezi kufanya kazi pamoja naye ikiwa sisi ni walegevu na wazembe.  Tukitaka atutumie hatuna budi nasi kuwa wachapakazi kama wakulima.  Mkulima kijijini huamka alfajiri na kwenda shambani na kurudi usiku, na kuchapa kazi kwa jasho na kula chakula kidogo tu.  Hatuna budi kuchapa kazi hivi ikiwa tunataka makanisa yetu yaongezeke au Zoni, Seksheni, au Makanisa yetu ya Nyumbani.  Afanyaye kazi ya Bwana kwa ulegevu, amelaaniwa (YEREMIA 48:10; WARUMI 12:11).

(3)                          SISI NI MATAWI (MST. 5)
Watu tuliookolewa, ni matawi ya Mzabibu wa Kweli.  Yesu Kristo ndiye mizizi na shina.  Kutoka kwake tunapata uzima.  Chakula, maji na madini mengine hutoka chini kwenye mizizi na kupanda juu kwenye matawi.  Uzima au uhai wetu unatokana na Yesu.  Wokovu wetu hutoka kwake.  Ikiwa tawi linaonekana kijani kibichi linapendeza, kupendeza huko hutokana na mizizi.

(4)                          KILA TAWI LINAPASWA KUZAA MATUNDA (MST. 2)
Mungu anamtazamia  kila Mkristo kuzaa matunda ya Ukristo, matunda yapasayo toba, matunda ya haki (MATHAYO 3:8; WAFILIPI 1:10-11; WAKOLOSAI 1:10).  Maisha yetu, hayana budi kuonyesha kwamba tumetubu dhambi zetu na kuziacha.  Ikiwa tunafanya yaleyale tuliyokuwa tukiyafanya kabla ya kutubu dhambi zetu, hiyo inaonyesha kwamba sisi ni matawi yasiyozaa matunda.  Hatuna budi kuonyesha matunda katika usemi, mwenendo, upendo, imani na usafi (1 TIMOTHEO 4:12).  Siyo hilo tu, kila mtu aliyeokoka, anatazamiwa kuzaa matunda, yaani kuzaa watoto wa kiroho (1 WAKORINTHO 4:15).   Kama sisi tulivyoshuhudiwa na kuokolewa, sisi nasi, hatuna budi kuwashuhudia wengine, na kuonyesha matunda yetu, yaani watu waliookolewa katika huduma zetu kwa njia ya Injili.

(5)                          KUONDOLEWA KWA TAWI LISILOZAA (MST. 2, 6)
Mtu yeyote anayedai kwamba ameokoka, lakini hazai matunda tuliyojifunza; huyu ni tawi lisilozaa.  Hukatwa na kuondolewa, na kutupwa motoni.  Ili tupate uzima wa milele, hatuna budi kuishi wakati wote maisha yanayoonyesha matunda.

(6)                          KUSAFISHWA KWA TAWI LIZAALO (MST. 2)
Wakulima wa Mikahawa, huyaondoa matawi yasiyofaa katika mikahawa na kuyasafisha yaliyo mazuri ili yazidi kuzaa.  Kusafishwa kunakozungumzwa hapa ni kupogoa au kiingereza kufanya “PRUNING“.  Mungu wetu hufurahishwa sana na mtu yeyote aliyeokoka ambaye anazaa matunda.  Huyu, husafishwa, ili azidi kuzaa matunda.  Hupewa neema ya ziada ili azidi kuzaa matunda katika tabia yake ya Ukristo.  Mtu anayewaleta wengi kwa Yesu, hupewa karama mbalimbali ili zizidi kumfanya kuwaleta wengi zaidi.

(7)                          KUSAFISHWA KWA NENO LA MUNGU (MST. 3)
“Mmekwisha kuwa safi, kwa sababu ya lile NENO nililowaambia“.  Wanafunzi wa Yesu walikuwa wamekwisha kuokolewa, lakini walifanywa safi zaidi kwa Neno la Kristo.  Tunapookoka, ni mwanzo tu wa safari.  Tunakuwa bado hatujawa safi, kama inavyotupasa, ndiyo maana inatubidi kuhudhuria kila ibada Jumatatu, Jumatano, Jumamosi na Jumapili, na pia kusikiliza kaseti za mafundisho na kusoma biblia, ili tufanywe safi zaidi kwa Neno la Mungu.  Wanafunzi wa Yesu hapa walikuwa wamekwisha kukaa pamoja na Yesu kwa miaka MITATU na tayari walikuwa wamekwisha kuanza mwaka wa NNE.  Nyakati za Biblia, wana wa Israeli walipokaribia kuingia Kanaani, Mungu aliwapa Agizo kuhusu matunda, akasema, “Nanyi hapa mtakapoingia nchi ile, mkiwa mmepanda miti ya namna zote kwa ajili ya chakula, ndipo mtayahesabu matunda yake kama KUTOTAHIRIWA, muda wa MIAKA MITATU miti hiyo itakuwa kwenu kama kutotahiriwa; matunda yake hayataliwa.  Lakini MWAKA WA NNE matunda yake yote yatakuwa ni MATAKATIFU,  kwa ajili ya kumpa BWANA shukrani (MAMBO YA WALAWI 19:23-24).  Huu ulikuwa utabiri unaohusu wanafunzi wa Yesu.  Walikuwa wamekaa pamoja naye miaka mitatu katika hali ya kuwa kama wasiotahiriwa, na mwaka wa nne, ndipo wakahesabiwa kuwa safi.  Hapa tunajifunza kwamba tunapookolewa bado tunakuwa hatujatahiriwa miyo yetu.  Inatupasa kumwomba Mungu atutahiri mioyo yetu ili tuwe na mioyo safi na kuwa watakatifu (KUMBUKUMBU 30:6; WAKOLOSAI 2:11; WARUMI 2:29; MATHAYO 5:8).  Baada ya kutahiriwa mioyo yetu, ndipo tunapokuwa na sifa ya kuingia mbinguni.  Ni muhimu kukumbuka pia kwamba usafi wetu utategemea jinsi tunavyokuwa tayari kuchongwa kwa neno la Mungu.  Tukikwepa kuchongwa kwa Neno la Mungu, hatuwezi kuwa safi.

(8)                          PASIPO YESU SISI HATUWEZI KUFANYA NENO LOLOTE (MST. 4-5)
Ni muhimu wakati wote kukumbuka kwamba utoshelevu wetu watoka kwa Yesu (2 WAKORINTHO 3:5).  Sisi ni matawi.  Matawi yasipopata chakula na maji kutoka kwenye mizizi, hunyauka na kufa.  Uwezo wetu wa kufanya neno lolote, unatoka kwa Yesu aliye mizizi.  Bila yeye hatuwezi kufanya neno lolote.  Hapa neno halisemi bila Yeye hatuwezi kufanya NENO LOLOTE KUBWA, kama kufufua watu, kuponya walio na Ukimwi n.k., neno linasema hatuwezi kufanya neno lolote hata lililo dogo.  Katika yote, WAKATI WOTE, hatuna budi kuitumainia NEEMA ya Mungu na kamwe tusijitumainie wenyewe HATUWEZI! (2 WAKORINTHO 1:8-9; 12:9).

(9)                          SIRI YA KUJIBIWA MAOMBI (MST. 7)
Tukitaka kuona matokeo makubwa zaidi ya maombi yetu, hatuna budi kukaa ndani ya Kristo, yaani kuokolewa na kuwa viumbe vipya (2 WAKORINTHO 5:17).  Siyo hilo tu, maneno yake hayana budi kukaa ndani yetu kwa WINGI (WAKOLOSAI 3:16).  Neno la Mungu litatuwezesha kuifahamu KWELI yenye uwezo wa kutuweka huru mbali na uongo wa Shetani.

(10)                   KUZAA SANA HUMTUKUZA BABA (MST. 8)
Matendo yetu mema au mwenendo wetu mzuri katika wokovu, humtukuza baba yetu aliye mbinguni (MATHAYO 5:16; 1 PETRO 2:12).  Tukisema tumeokoka lakini maisha yetu yanakuwa hayako nuruni mbele ya mataifa; tunapigana na wake zetu na kutukanana, na kufanya mengi yaliyo kinyume na wokovu; watu hawa huona wokovu ni uongo na hivyo hawamtukuzi Baba yetu.  Tunapokuwa tunawashuhudia watu wengi na kuwaleta kwa Yesu, pia Baba yetu wa mbinguni hutukuzwa kwa jinsi ufalme wake unavyoongezeka.  Hatuna budi kukumbuka wakati wote amri takatifu tuliyopewa, “MTENDAPO NENO LOLOTE, FANYENI YOTE KWA UTUKUFU WA MUNGU“ (1 WAKORINTHO 10:31).

(11)                   KUZAA SANA, ALAMA HALISI YA MWANAFUNZI WA YESU (MST. 6)
Tunadhihirika kuwa sisi ni wanafunzi wa Yesu pale tu tunapozaa sana matunda katika mwenendo wetu na katika injili yetu.  Kinyume cha haya, madai yetu kwamba sisi ni wanafunzi wa Yesu, yanakuwa si ya kweli.
…………………………………………………………………………………………………………………………………..
Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni?  Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14).  Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).  Kinyonge ni kipi?  Ni yule anayetenda dhambi.  Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge!  Je, wewe ni mtakatifu?  Jibu ni la!  Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13;  YOHANA 14:6).  Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii?  Najua uko tayari.  Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni;  Mungu Baba asante kwa ujumbe huu.  Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi.  Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo.  Bwana Yesu niwezeshe.  Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu.  Amen.  Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni.  Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!
. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . 
Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “somo” hili, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe.

Post a Comment

0 Comments