Ticker

6/recent/ticker-posts

UNA NINI, EWE ULALAYE USINGIZI? AMKA UKAMWOMBE MUNGU by BISHOP KAKOBE


UNA NINI, EWE ULALAYE USINGIZI? AMKA UKAMWOMBE MUNGU


ZACHARY KAKOBENeno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        
Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org

SOMO LA 9: UNA NINI, EWE ULALAYE USINGIZI?  AMKA UKAMWOMBE MUNGU

NENO LA MSINGI:
YONA 1:6
“Basi nahodha akamwendea, akamwambia, UNA NINI, EWE ULALAYE USINGIZI? AMKA UKAMWOMBE MUNGU wako; labda Mungu huyo atatukumbuka tusipotee”.
<><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><>> 
M
tu aliyeokoka anapokuwa mvivu na kupenda usingizi tu kuliko kufanya maombi, mtu huyu anasababisha bahari yake ya kiroho kuchafuka na kuleta misukosuko mingi na hatari ya roho yake.  Shetani kama simba aungurumaye, anazunguka huko na huko akitafuta mtu mvivu anayependa usingizi ili ammeze.  Shetani hasinzii, anakesha kama mwizi akivizia watu wanaolala na kusahau umuhimu wa kumwomba Mungu.  Akiwapata hao, huwaibia nguvu yao ya kiroho na kuwameza, kwa kuwaingiza katika utawala wake.  Shetani hatulii kamwe.  Wakati wote huzunguka na kutembea huku na huku kutafuta watu waliookoka waliolala usingizi na kuacha kumwomba Mungu ili awameze:

AYUBU 2:2
“Bwana akamwuliza Shetani, Umetoka wapi?  Shetani akajibu Bwana, na kusema, Natoka katika kuzunguka-zunguka duniani, na katika kutembea huku na huku humo.”

I PETRO 5:8
MWE NA KIASI NA KUKESHA:  Kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye huzunguka – zunguka, akitafuta mtu ammeze.”

NINI MAANA YA KUWA NA KIASI NA KUKESHA?

1.         KUKESHA
Kukesha kunakozungumzwa hapa, siyo kutokulala usingizi usiku siku zote, Mtu anaweza akawa hajalala usingizi usiku mzima, lakini akawa hajakesha katika maana ya ki-biblia.  Inaweza ikawa saa moja lakini ikaitwakukesha.  Angalia maandiko:
MATHAYO 26:40;
“Akawajia wale wanafunzi, akawakuta wamelala, akawaambia Petro, Je! hamkuweza KUKESHA PAMOJA NAMI HATA SAA MOJA?”
Unaona ‘kukesha siyo tu suala la kukaa macho usiku kucha’  Maana ya kukesha ki-Biblia ni kujihadhari kabla ya hatari kwa kuivaa silaha ya maombi tayari kwa vita na adui.

KUTOKA 3:18
“…….Wana wa Israeli wakakwea kutoka nchi ya Misri hali wamevaa silaha.”
Huku ndiko kukesha, tunakwenda Kanaani huku tukiwa tumevaa silaha ya maombi.  Kukesha lazima kuambatane na maombi.  Siyo kuimba pambio mpaka kutoka jasho.  Kuimba sana pambio siyo kukesha.  Kushuhudia wakati wote jinsi ulivyookoka miaka kumi na tano iliyopita siyo kukesha.  Mtu anayekesha ni mtuanayeomba,yaani anayewasiliana na Mungu.  Shetani anapozunguka zunguka na kumkuta mtu ambaye ana maisha ya maombi, anaogopa hata kumkaribia; kwa sababu anajua hawezi kummeza mtu huyo.  Silaha ya maombi ni silaha kubwa mno kuliko silaha yoyote ya majeshi ya Ibilisi na hivyo Shetani anapomuona mtu aliyeokoka amevaa silaha hiyo, huogopa mno na akituma majaribu yake, hayawezi kummeza mtu huyo. Mtu mwombaji, hawezi kuingia majaribuni bali yeye siku zote hupita katika majaribu na kuyashinda.  Kuna tofauti kati ya kuingia majaribuni na kupita katika majaribu.

(a)       KUPITA KATIKA MAJARIBU
Kupita katika majaribu ni kukabiliana na majaribu na kuyashinda kama vile wana wa Israeli walivyopita kati ya Bahari ya Sham wakati wa Musa, na tena walivyopita kati ya Mto Yordani ulipokuwa umefurika na maji hayakuwafikia kabisa [SOMA KUTOKA 14:22; YOSHUA 3:15-17]. Inawezekana tu kupita katika majaribu tunapokuwa watu wa maombi.  Mtu anayeomba hawezi kufikiwa na maji yaliyofurika.

ZABURI 32:6
“Kwa hiyo kila mtu mtauwa (Mtakatifu) akuombe wakati unapopatikana.  Hakika maji makuu yafurikapo, hayatamfikia yeye”.

(b)       KUINGIA MAJARIBUNI
Kuingia majaribuni, ni kumezwa na jaribu na ukashindwa.  Maji yafurikapo, lazima yatammeza kabisa mtu asiyekuwa mwombaji.
MATHAYO 26:41:
Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribuni…………………….”.

Mtu yeyote asiyekuwa mtu wa maombi ni mtu aliyelala.  Mtu huyu hakeshi, na lazima atamezwa na shetani anayezunguka-zunguka akitafuta watu waliolala ili awameze.  Mtu asiyeomba ni mtu ambaye amelala na kuivua silaha yake, na kuiweka mbali naye.  Shetani anapokuja, anamkuta hana silaha yoyote na hivyo anammeza kirahisi.  Anakuwa ameingia majaribuni.  Mtu mwenye silaha hupita katika majaribu kwa kuyashinda na kuyaacha nyuma.

(2)       KUWA NA KIASI
Kuwa na kiasi ni kuwa na nidhamu ya kujipangia utaratibu wako ambao utahakikisha kwamba shughuli za ulimwengu huu hazikufanyi usahau kumwomba Mungu.  Kinyume cha kiasi, ni kulemewa.  Ukilemewa na masumbufu ya maisha haya na kukosa muda wa kukesha hata saa moja katika  maombi kila siku, ujue shetani na majeshi yake yatakumeza tu.

LUKA 21:34
“Basi, jiangalieni, mioyo yenu isije ikalemewa na ……….. masumbufu ya maisha haya;siku ile ikawajia ghafula, kama mtego unasavyo.”

Mtu aliyeokoka mwenye kuwa na kiasi na kukesha ndiye mtu atakayepita katika majaribu na kuwa miongoni mwa wale washindao.  “Yeye ashindaye nitampa kuketi pamoja nami katika kiti changu cha enzi kama mimi nilivyoshinda…..” [UFUNUO 3:21]  Yesu alishinda kwa sababu alikuwa mwenye kiasi na kukesha.

JITAHIDI KATIKA MAOMBI
Kuwa mtu wa maombi, kunahitaji jitihada.  Pasipo kujitahidi na kudhamiria kabisa kuwa mtu wa maombi, huwezi kuwa mtu wa maombi.
WARUMI 15:30:
“Ndugu zangu, nawasihi kwa Bwana wetu Yesu Kristo, na kwa upendo wa Roho, JITAHIDINI PAMOJA NAMI KATIKA MAOMBI YENU…………….”

Ni rahisi kuhubiri na kufundisha lakini siyo rahisi kuomba.  Ni rahisi kuimba pambio za sifa lakini siyo rahisi kuomba.  Mitume wale kumi na wawili wa Yesu hapo mwanzo, walikuwa wanahubiri na kufundisha [MARKO 6:12;30] na tena walikuwa hodari wa kuimba.  Waliimba pambio za sifa pamoja na Yesu mwenyewe [MARKO 14:26] lakini pamoja na hayo yote, hawakuweza kukesha hata saa moja.  Matokeo yake ni kwamba wangeweza kupepetwa na shetani kama ngano wakati wowote.
Kipimo cha kiroho cha mtu, ni jinsi gani alivyo mtu wa maombi na siyo jinsi gani anavyoweza kuimba au kuhubiri na kufundisha.
Inahitaji kabisa kudhamiria kuomba; Au siyo, utavutwa zaidi kufanya mazungumzo yasiyo na maana yoyote kwa masaa mengi kuliko kuomba saa moja.  Utasingizia uchovu wa kazi, lakini pamoja na uchovu huo; unaweza kuzungumza na watu mpaka usiku wa manane, lakini huwezi kuzungumza na Mungu saa moja.  Pamoja na uchovu huo, unaweza ukasoma gazeti moja baada ya jingine kwa masaa mengi; lakini huwezi kumwomba Mungu.

Ili uwe mtu wa maombi inakubidi ujitahidi kabisa kuutiisha mwili wako na kuukatalia furaha zake za kimwili kama kulala usingizi, kupenda tu kuongea n.k. na uufundishe kuomba.  Ni lazima kabisa uwe na uwezo wa kuitawala roho yako na kuifanya iwe na kiasi katika masumbufu ya dunia, na ipende kukesha; au siyo unakuwa mfano wa mji uliobomolewa, usio na kuta ambao shetani anaweza kuingia tu apendavyo.

MITHALI 25:28:
” Asiyetawala roho yake ni mfano wa mji uliobomolewa, usio na kuta.”

DALILI KUMI NA MOJA (11) ZA DHAHIRI, ZA MTU ALIYEKWISHA KUINGIA MAJARIBUNI, NA KUMEZWA NA SHETANI KWA KUKOSA KUWA NA
KIASI NA KUKESHA

1.         Kuanza kukosa kuhudhuria kusanyiko la Kanisa la Nyumbani na ibada za Kanisa Kuu kwa visingizio mbalimbali, huku dhamiri yako haiumii; na ukaanza kuwaza moyoni kwamba hata ukijisomea Biblia mwenyewe nyumbani inatosha [WAEBRANIA 10:25].
2.         Kuanza kufuata njia zako mwenyewe tofauti na jinsi ulivyojifunza katika mafundisho ya Neno la Mungu [MITHALI 14:14a].
3.         Kuanza kufanya mazoea ya kwenda Kanisani na kusikia Neno la Mungu lakini hakuna hatua yoyote ya kulitii na kulitenda.  Kuanza kuona Neno la Mungu kama wimbo tu.
[EZEKIELI 33:30-32].
4.         Kuanza kukataa maonyo ya Mchungaji kwa kujiona kuwa umekua sana kiroho, na eti mshauri wako ni Roho Mtakatifu na Yesu peke yao! [MHUBIRI 4:13].
5.         Kuanza kuzifuata njia za mataifa katika mavazi, usemi na matendo mengine; na kusema   moyoni kwamba Mungu anaangalia roho tu, haangalii mwili [WARUMI 12:2;
2 WAFALME 17:5].
6.         Kuanza kuipenda dunia na kusongwa na kutafuta nguo, mali, elimu, vitu, anasa, n.k. na kuvipa umuhimu wa kwanza kuliko kumtafuta Mungu [I YOHANA 2:15;I TIMOTHEO 6:9-10].
7.         Kuanza kutokuona umuhimu wa kuzipitia “Notes” za mafundisho ya Kanisa unapokuwa Nyumbani, na kuyachunguza maandiko zaidi katika Biblia na kuona kwamba inatosha tu Kanisani [MATENDO 17:11].
8.         Kutokana na kuongezeka katika kulijua Neno la Mungu [WAEBRANIA 5:12].
9.         Kuanza kuona ya kwamba huna haja ya kuongozwa, na kuwaka tamaa ya kutaka kuwa kiongozi na kusema kila mmoja anaweza kujiongoza mwenyewe maana wote tuko sawa [HESABU 16:1-3, 8-10].
10.       Kuanza kuona kwamba maombi, kusoma Neno, kufanya kazi ya Mungu ni mambo yasiyofurahisha [UFUNUO 2:4-5; WAEBRANIA 3:14].

11.       KUANZA KUONA dhambi ni kitu cha kawaida, na kuona ni kawaida kusema uongo na kusengenya na kuanza kutenda dhambi nyingi kisirisiri ukijionyesha kuwa u mtakatifu mbele ya watu waliookoka na dhamiri haikushuhudii kutubu na kuacha [UFUNUO 3:1].
Kanisa kama limejaa watu wasiokuwa na kiasi na kukesha, Kanisa hilo halikujengwa kwenye Mwamba na ni dhahiri kwamba milango ya kuzimu italishinda.  Mwamba Yesu Kristo, alikuwa mwenye kuwa na kiasi na kukesha.  Kama kanisa limejengwa kwenye msingi wake, litakuwa na watu wa maombi.

AINA YA MAOMBI YANAYOITWA MAOMBI YA KUKESHA

Maombi ya kukesha ni yale yanayohusiana na vita ya kiroho.  Vita vyetu siyo vya kimwili bali vya kiroho [WAEFESO 6:12].  Ni vyema kuomba juu ya mahitaji binafsi ya kimwili tuliyo nayo, lakini hayo hayaitwi maombi ya kukesha.  Kuomba mchumba, cheo, nyumba, chakula, nauli, nguo, gari n.k; siyo maombi ya kukesha.  Wanafunzi wa Yesu walikuwa na maombi ya kibinafsi lakini hawakuwa wakikesha hata saa moja [MARKO 10:35-37].  Maombi ya kukesha ni kuomba juu ya kulijua Neno zaidi; nguvu zaidi za kumtumikia Mungu; kuomba neema zaidi ya kuwa mwombaji; kuomba neema zaidi ya kielelezo cha utakatifu ofisini, kiwandani, katika kazi na biashara na za majirani; kuomba neema zaidi ya kulitii Neno na kulitenda; kuomba kwa ajili ya watu kuokolewa na kuongezeka kwa Kanisa la Mungu; kuomba ongezeko la watu katika Kanisa la Nyumbani na Kanisa Kuu; kuomba kwamba wale wasiopenda mafundisho na waliorudi nyuma katika wokovu waamshwe na Roho na kuanza upya kumpenda Yesu na Neno lake; kuomba neema zaidi kwa Mchungaji; kuomba kwa ajili ya Uongozi wa Roho wa Mungu katika kufanya mambo yote katika Kanisa; kuomba kwa ajili ya watu katika Kanisa wazidi kujitoa katika kumtumika Mungu kwa mali zao, muda wao, nguvu zao n.k; kushindana na nguvu za giza zilizo kinyume na kuenea kwa kweli ya Neno la Mungu katika Taifa, ulimwengu, n.k; kuomba kwa ajili ya mikutano na huduma mbalimbali za kanisa; Kuomba kwa ajili ya mahitaji ya fedha ya kutendea kazi ya Mungu katika kanisa n.k; Haya ndiyo maombi ya kukesha.

BAHARI KUCHAFUKA
“Jijaribuni wenyewe kwamba mmekuwa katika imani, jithibitisheni wenyewe……..”
[2 WAKORINTHO 13:5].  Je wewe hujamezwa na shetani kwa kutokuwa na kiasi na kukesha?  Hakuna dalili mojawapo katika kumi na moja zilizotajwa ambayo inakusema mwenyewe?  Je wewe ni mkeshaji au unapenda usingizi tu?  Huenda bahari imechafuka katika Kanisa la Mungu kwa sababu yako uliyelala.  Amka leo na uanze upya kumwomba Mungu katika maisha yako.  Ikiwa umekwisha mezwa na kuingia majaribuni, tubu na kumwomba Mungu akuokoe na yule mwovu na umwahidi kuanza upya leo.

YONA 1:6:

“Basi nahodha akamwendea, akamwambia, UNA NINI, EWE ULALAYE USINGIZI?  AMKA UKAMWOMBE MUNGU WAKO, labda Mungu huyo atatukumbuka tusipotee.”

M   A   S   W   A   L   I

1.         Nini maana ya kukesha?
—————————————————————————————————————-
—————————————————————————————————————-
2.         Nini maana ya kuwa na kiasi?
—————————————————————————————————————-
—————————————————————————————————————-
3.         Nini tofauti ya kuingia majaribuni na kupita katika majaribu?
—————————————————————————————————————
—————————————————————————————————————-
4.         Kuomba kunahitaji jitihada na kudhamiria.  Umepanga kufanya nini ili uwe mwombaji kuanzia leo?
—————————————————————————————————————-
—————————————————————————————————————-
5.         Kipimo cha kiroho cha mtu ni nini?
—————————————————————————————————————-
—————————————————————————————————————-
—————————————————————————————————————
6.         Mtu asiyeitawala roho yake na kuwa na kiasi akiomba, amefananishwa na nini na hasara yake ni nini? [MITHALI 25:28].
—————————————————————————————————————-
—————————————————————————————————————-
—————————————————————————————————————-
<><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><>< 
Usikose faida zilizomo katika somo lililotangulia “NITATUMAINI WALA SITAOGOPA”, ingia hapa ujifunze Neno la Mungu<> https://davidcarol719.wordpress.com/nitatumaini-wala-sitaogopa/                                       ><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><>< 
Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni?  Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14).  Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).  Kinyonge ni kipi?  Ni yule anayetenda dhambi.  Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge!  Je, wewe ni mtakatifu?  Jibu ni la!  Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13;  YOHANA 14:6).  Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii?  Najua uko tayari.  Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni;  Mungu Baba asante kwa ujumbe huu.  Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi.  Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo.  Bwana Yesu niwezeshe.  Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu.  Amen.  Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni.  Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!
. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . 
Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “note” hii, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe.
                                                         UBARIKIWE NA BWANA YESU!
<><><><><><><><><><><><><><><><><><><>><><><><><><><><><><><><><><>

Post a Comment

0 Comments