Ticker

6/recent/ticker-posts

Ufugaji wa Nyuki Wapunguza Umaskini, Watunza Mazingira


Marko Gideon 

DAR ES SALAAM, FEB 15 (IPS) - Ufugaji wa nyuki katika maeneo mengi ya Tanzania unafanyika kuzalisha kipato, lakini kwa jumuiya za pwani, ufugaji huo una madhumuni makuu mawili – kuingiza kipato na kuhifadhi mazingira. 

Mzee Athmani Salim, mmoja wa wakazi wa kijiji cha Mkalamo wilayani Pangani, anakiri kuwa ufugaji wa nyuki ni miongoni mwa shughuli muhimu sana katika kumwingizia kipato na hivyo kumudu kuendesha maisha yake, ikiwa ni pamoja na kuwa na uwezo wa kukabiliana na matatizo mbalimbali ya kiafya na kifamilia.

Mzee Salim anasema kuna wakati alipatwa na maradhi hatari mno katika umri wake unaokadiriwa kuwa katika miaka ya 50 hadi 60, ambayo yangetishia uhai wake kama asingekuwa na kiasi cha fedha kilichohitajika kuyatibu.

"Baada ya kugundulika na ugonjwa huo, niliambiwa na tabibu kuwa maradhi yale yasingeweza kutibiwa kama nisingelipa zaidi ya shilingi 650,000, lakini sikuwa na wasiwasi kwasababu nilikuwa na fedha za kutosha zilizotokana na kipato cha kuuza asali iliyotokana na ufugaji wa nyuki," anasema huku akionyesha uso wa tabasamu.

"Sasa niko fiti, na hali isingekuwa hivyo kama nisingekuwa na kipato kilichotokana na ufugaji wa nyuki," aliongeza na kushangiliwa na wanakijiji wenzake waliokusanyika katika shule ya msingi Mkalamo wakati wa tathmini ya mafanikio ya shughuli zinazoendeshwa na Mradi wa Ushirika wa Kusimamia Mazingira na Rasilimali za Pwani na Bahari (TCMP Pwani), unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani na kupata msaada wa kiufundi kutoka Kituo cha Rasilimali za Bahari cha Chuo Kikuu cha Kisiwa cha Rhode.

Kama ilivyo kwa wanakijiji wengi wa Mkalamo, mzee Salim anamiliki mizinga kadhaa binafsi ya kienyeji na mingine ya kisasa na ni mjumbe wa kikundi cha ufugaji wa nyuki kinachopatiwa msaada na TCMP Pwani.

Kwa mujibu wa mzee huyo, kutokana na uhaba wa mvua, katika mavuno ya hivi karibuni alipata ndoo 4 tu za asali zenye ujazo wa lita 20. Kiasi hiki ni sawa na jumla ya lita 80 ambazo kila lita huuzwa kwa shilingi 8000.

Kipato hiki siyo haba kwa taifa ambalo wananchi wake wengi, hasa wale wanaoishi maeneo ya vijijini wanaishi chini ya dola moja kwa siku. Kwa mujibu wa utafiti wa bajeti katika ngazi ya kaya wa mwaka 2007, asilimia 34 ya Watanzania, hasa katika maeneo ya vijijini, wanaishi chini ya umaskini wa kuweza kupata mahitaji ya lazima.

Pia kiwango hiki cha uzalishaji siyo kidogo, katika taifa ambalo linatumia asilimia 4 tu ya fursa zilizopo za uzalishaji wa asali.

Alipokuwa akifunga maonesho ya miaka 50 ya uhuru ya wizara, idara na taasisi za serikali Desemba 12, 2012, Waziri Mkuu, Mizengo Peter Pinda, alisema "Tanzania inatumia fursa ya uzalishaji wa asali kwa asilimia 4 tu. Asilimia 96 ya fursa hiyo haitumiki". Alisema Ethiopia ni nchi inayoongoza kwa uvunaji wa asali katika bara la Afrika.

Takwimu zinaonyesha pia kuwa Ethiopia ni miongoni mwa mataifa 10 bora kwa uzalishaji wa asali duniani na kati ya mataifa 5 yanayoongoza katika uzalishaji wa nta. Tanzania ingeweza kutumia fursa zilizopo pengine ingeweza kuipiku hata nchi ya Ethiopia kwa uzalishaji wa asali na mazao mengine yanayotokana na ufugaji wa nyuki.

Faida za ufugaji wa nyuki

Ufungaji wa nyuki, kwa kiasi kikubwa, unalenga katika kuzalisha asali ambayo ina faida nyingi kwa wananchi. Kwa mujibu wa wanakijiji wa Mkalamo, Asali hutumika kama chakula, hutumika kama dawa, hutumika kuinua uchumi wa familia na wa jamii kwa ujumla.

"Asali bwana ina manufaa mengi. Moja ni chakula; watoto wakila wakinywa maji, hawaoni njaa tena," alisema mzee Salim. "Ukichanganya na unga wa dona - lita moja na kilo moja ya unga halafu uikoroge pamoja halafu na kuifunika pembeni kwa siku tatu, inakuwa mkate, ukikata kipande halafu ukimpa mtoto akala, kutwa atakuwa akinywa maji, hatakusumbua tena."

Asali ni tiba ya vidonda vya tumbo, inaongeza damu kwa asiyekuwa na damu na inaponyesha madonda ndugu, kwa mujibu wa mzee Salim.

"Hata nilipokuwa nimelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Pangani nilienda na lita zangu kama tano, basi ziliishia pale pale hospitalini. Kumbe madaktari walikuwa wakiitumia walipokuwa wakifanyia operesheni akina mama wajawazito," alisema mzee huyo.

Mzee Salim ambaye kikundi chake cha ufugaji wa nyuki cha Lukundembara kinachomiliki eneo la ekari 50 na kumiliki mizinga 35, na yeye mwenyewe kuwa na mizinga 92 na wake zake wawili, kila mmoja akimiliki mizinga 10, anaelezea zaidi juu ya faida za ufugaji wa nyuki. "Ufugaji wa nyuki umenisaidia na sasa ukulima wangu unatumia trekta kwa sababu ya asali. Vijumba vyangu vya makuti sasa navibadili ili kuwa vya bati".

Mbali ya faida za asali zinazotokana na ufugaji wa nyuki, zao jingine linaloweza kuongeza kipato kwa wafugaji wa nyuki ni nta.

Wanajamii wa Mkalamo wanakiri kuwa vipato vyao vimeongezeka kutokana na kupata mafunzo ya utengezaji wa nta na hatimaye nta kutengeneza mishumaa kutoka kwa wataalam wa TCMP Pwani.

Hifadhi ya mazingira

Kwa mujibu wa Rukia Seif, Mhamasishaji Kata wa Shughuli za Vikundi vya Maendeleo vya Mradi wa TCMP Pwani katika Kata ya Mkalamo yenye vijiji viwili ambavyo ni Mkalamo yenyewe na Mbulizaga, wafugaji nyuki pia husaidia kuhifadhi mazingira kwa kutundika mizinga kwenye misitu hivyo wanakijiji kushindwa kuvamia misitu ambayo imetundikwa mizinga hiyo. Wavamizi wakorofi wanaovamia misitu hiyo hukabiliana na wafugaji wa nyuki.

Hili ndilo lengo kuu la Mradi wa TCMP Pwani, kuwezesha wananchi wanaoishi katika mwambao wa bahari kuwa na shughuli za uzalishaji kipato ambazo aidha ni rafiki wa mazingira ama zitawahamasisha kutunza mazingira.

Njia mbadala za uzalishaji kipato pia hupunguza hali ya kutegemea kwa kiasi kikubwa rasilimali za pwani na bahari, ambazo kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu na sababu nyingine, zimeanza kupungua na hivyo kutishia kuwa endelevu.

Pia TCMP Pwani ilitoa mafunzo, msaada wa kusajili na kuanzishwa kwa Kikundi cha Kuweka na Kukopa (SACCOS) kwa lengo la kupata mtaji wa kuanzisha shughuli mbadala za uzalishaji mali kwa kuzingatia utunzaji wa mazingira.

Kwa mujibu wa Hashim Mwisongo, mwenyekiti wa kijiji cha Mkalamo na katibu wa SACCOS na kikundi cha ufugaji wa mbuzi wa maziwa, "kusudi na malengo yetu ni kwamba hawa watu tunawashawishi kuhifadhi mazingira. SACCOS imeingia mkataba na TCMP kuwa wanachama wote wanaojiunga na SACCOS hawajihusishi na uharibifu wa mazingira".

Uhaba wa mvua hupunguza uzalishaji wa asali

Mavuno ya asali mara nyingi yanategemeana na hali ya kunyesha kwa mvua katika eneo husika. Kwa mujibu wa Elizabeth Emanuel kutoka kijiji cha Mbulizaga "nina mizinga binafsi 18, napata debe 3 hadi 4 kulingana na hali ya mvua".

Kwa mujibu wa mama huyo ambaye alisema tofauti na mazao mengine, soko la asali halina wasiwasi kwani huuza asali palepale nyumbani kwa shilingi 8000 kwa lita, hali ya kukosekana kwa mvua ni changamoto kubwa kwa uzalishaji wa asali.

"Ufugaji wa nyuki una faida kubwa. Napenda nisonge mbele, hivi sasa najitahidi kununua mizinga ili iweze kuongezeka zaidi, napenda nisonge mbele nifikishe hata mizingi 200," anasema. "Lakini changamoto ni kwamba, kama mvua ni chache, hupati mavuno mengi, unapata kiasi tu. Lakini mvua inapokuwa nyingi asali inaongezeka".

Maneno yake yanaungwa mkono na mzee Salim ambaye anasema nyuki wanahitaji maji, maji yanapokosekana, huwezi kupata nyuki katika mizinga yako. Nyuki wanaweza kukimbia mizinga kama kunakuwa na ukame, kunakosekana maji, na uoto wa asili unapotoweka. (END/2012)

Post a Comment

0 Comments